Tuesday, October 18, 2016

Meneja Mkuu Mpya akutana na Watumishi wa Shirika

 Katika picha ni sehemu ya Watumishi wa Shirika la Masoko  Kariakoo wakiwa wanamsikiliza Meneja Mkuu mpya wa Shirika hili. Meneja Mkuu huyo mpya aliitisha mkutano huu ili aweze kujitambulisha kwa Watumishi wa Shirika. Bwana Hetson Msalale Kipsi pichani hayupo aliteuliwa rasmi na Mheshimiwa Rais Dk.John Magufuli tarehe 5 Septemba 2016 kuwa Meneja Mkuu Mpya wa Shirika hili. Bwana Kipsi kabla ya uteuzi huo alikuwa Mtumishi katika Wizara ya TAMISEMI, kwa taaluma yeye ni Mtaalam wa  Mambo ya Uchumi.
 Katika picha hapo juu ni Wajumbe wa Menejimenti ya Shirika la Masoko Kariakoo waliokaa mbele. Kutoka kushoto ni Meneja wa Fedha Bi.Marieta Masaua, Bwana Mathias Mbafu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, Bwana Donald T.Sokoni ambaye ni Meneja wa Afya na Usafi, Bwana Josam Mnzava ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama na Mlelo Mghen huyu ni Meneja Mipango na Biashara. Hawa pia walijumuika katika mkutano huu maalum uliokuwa na lengo la kumtambulisha Meneja Mkuu Mpya wa Shirika Bwana Hetson Msalale Kipsi.
 Meneja Utumishi na Utawala Bwana Godwin Mrosso aliyesimama, akizungumza kumkaribisha Meneja Mkuu Mpya wa Shirika  Bwana Hetson Msalale Kipsi aliyekaa katikati ili aweze kuzungumza na Watumishi wa Shirika na kujitambulisha kwa Watumishi hao. Mkutano huo ulifanyika ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Shirika ulioko katika Jengo Kuu la Soko kuu la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam.
 Bwana Denis Mfuruki aliyesimama katika picha hapo juu ambaye ni Mwenyekiti wa TUICO Tawi la Shirika la Masoko Kariakoo, akizungumza kumkaribisha Meneja Mkuu Mpya Bwana Hetson Msalale Kipsi ambaye amekaa. Bwana Mfuruki alimshukuru na kumpongeza  Meneja Mkuu huyo mpya kwa ujio wake kama Mtendaji Mkuu wa Shirika na kwamba Watumishi wapo tayari kushirikiana naye ili kuliletea Shirika maendeleo.
 Bwana Ncheye Kulwa aliyesimama ambaye kwa nafasi yake katika Utumishi katika Shirika  ni Mkaguzi wa Ndani,alikuwa miongoni mwa Watumishi waliopata nafasi yakumueleza Meneja Mkuu Mpya baadhi ya kero ambazo zinawasibu Watumishi. Bwana Ncheye Kulwa alieza kuhusu maslahi duni kwa Watumishi hasa kuhusu mishahara kuwa ni midogo sana na kumuomba Meneja Mkuu huyo mpya kuliangalia jambo hilo ili Watumishi wa Shirika wapate maslahi mazuri.
 Sehemu ya Watumishi wa Shirika la Masoko Kariakoo waliohudhuria Mkutano maalum huo wa Meneja Mkuu mpya kujitambulisha rasmi kwa Watumishi wa Shirika. Aliyesimama ni Bwana Nicodemas Mwakalindile yeye kama miongoni mwa Watumishi wa Shirika alimshukuru na kumpongeza Meneja Mkuu huyo mpya kwa kuteuliwa kwake kuwa Meneja Mkuu mpya wa Shirika la Masoko Kariakoo. Pia alitoa kero yake mbele ya Meneja Mkuu mpya ya kuwa ndani ya Taasisi hii upendo baina ya Watumishi wa kada ya chini na Menejimenti umepungua sana na kumuomba Meneja huyu mpya aweze kuirekebisha hali hiyo ili watumishi waweze kuwa na morali ya kufanya kazi.
 Katika picha hapo juu, aliyesimama ni Bi.Romana Lukanga, Mtumishi huyu mkongwe katika Shirika la Masoko Kariakoo.Kihistoria Mama huyu aliajiriwa Mwaka 1975, na wakati Soko Kuu la Kariakoo lilipokuwa linafunguliwa na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K.Nyerere yeye alishuhudia tukio hilo. Mtumishi huyu ombi lake kubwa kwa  Meneja Mkuu mpya ni kumtaka aboreshe maslahi ya Watumishi wote hasa wale wa kada ya chini ndani ya Shirika hili.Akizungumza kwa hisia Mtumishi huyu Bi.Lukanga alimwambia Meneja Mkuu kuwa yeye pamoja na wenzake wa kada yake wamekuwa katika hali duni kwakuwa mishahara yao ni midogo sanaa ukilinganisha muda ambao wamelitumikia Shirika.
 Katika picha hapo juu ni Bwana Mdami ambaye Mtumishi wa Shirika kutoka Kitengo cha Matunzo. Bwana Mdami naye alisisitiza juu ya kuboreshwa maslahi ya Watumishi. Akimuomba Meneja Mkuu mpya aweze kurekebisha hali duni ya mishahara kwa Watumishi wa Shirika.
 Meneja Mkuu mpya Bwana Hetson Kipsi akiwa amesimama kujibu baadhi ya hoja ambazo zilizungumzwa na Watumishi wa Shirika, pale alipotoa nafasi kwa Watumishi kuzungumza dukuduku zao. Pamoja na mengine Meneja Mkuu aliwaahidi Watumishi wa Shirika kwamba masuala yao yote yatafanyiwa kazi ipasavyo kwa kuzingatia Sheria,taratibu na kanuni za Utumishi ambazo zimewekwa kuliendesha Shirika hili.Akizungumza na Watumishi hao katika Ukumbi wa mikutano wa Shirika Meneja Mkuu alikiri kuwa zipo baadhi ya kero na changamoto ambazo alizifahamu tangu mapema hata kabla hajafika kuanza kazi rasmi ndani ya Shirika hili, hivyo basi Watumishi waondoe shaka na kwamba yeye amekuja kufanya kazi na kila Mtumishi kwa mujibu wa Sheria na kanuni za Shirika.
 Hapo juu katika picha ni Bwana Godwin Mrosso Meneja Utumishi na Utawala wa Shirika, akijibu baadhi ya hoja zinazohusu mambo ya Utumishi na Utawala. Bwana Mrosso alipewa nafasi hiyo yakutoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja ambazo Watumishi walizitoa mbele ya Meneja Mkuu aliyekaa katikati.
 Aliyesimama katika picha hapo juu ni Bwana Charles Sombe ambaye ni Afisa Utumishi Mwandamizi katika Shirika la Masoko Kariakoo. Afisa huyu alitoa ushauri kwa Meneja Mkuu huyo kuondoa makundi au matabaka ambayo yapo ndani ya Shirika kutokana na tofauti kadhaa wa kadhaa ili kujenga upya mshikano miongoni mwa Wafanyakazi wa Shirika.
Katika picha hapo juu ni Bwana Josam Mnzava  Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama akifafanua jambo katika mkutano Maalum wa Watumishi wa Shirika la Masoko Kariakoo. Mkutano huo uliokuwa na Agenda moja tuu ya Meneja Mkuu Mpya wa Shirika hilo Bwana Hetson Msalale Kipsi kujitambulisha na kuwatambua Watumishi wa Shirika hili rasmi tangu alipoteuliwa na Rais mwezi mmoja uliopita na kuanza kazi rasmi mapema mwanzoni mwa mwezi huu akiwa ametokea katika Wizara ya TAMISEMI iliyoko chini ya Ofisi ya Rais.