Saturday, January 28, 2017

Ujumbe kutoka TAMISEMI na Jiji la DSM wakutana na Menejimenti ya Shirika

 Picha ya pamoja miongoni mwa Wajumbe waliohudhuria kikao cha kujadili mstakabali wa Shirika la Masoko ya Kariakoo. Miongoni mwao ni Kaimu Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa kutoka TAMISEMI Bi.Mirium Mmbaga aliyevaa vazi la Kitenge.
 Picha ya pamoja miongoni mwa wajumbe waliohudhuria kikao maalum kilichojadili juu ya mwenendo mzima wa kiutendaji wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, pamoja na Viongozi kadhaa kutoka TAMISEMI na Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam, pia ilikuwepo Menejimenti ya Shirika hili iliyoongozwa na Meneja Mkuu wa Shirika Bwana Hetsoni Msalale Kipsi mwenye suti nyeusi.
Katika picha hapo juu ni miongoni mwa Wajumbe wa kikao maalumu ambacho kilifanyika katika Ukumbi wa Shirika la Masoko Kariakoo wiki iliyopita. Kutoka kushoto wa kwanza  ni Bwana Eustard  Ngatale Mkurugenzi Msaidizi katika masuala ya Sheria kutoka TAMISEMI,Bwana Denisi Mfuruki yeye ni Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Masoko Kariakoo,watatu ni Bi.Miriam Mmbaga ambaye ni Mkurugenzi kutoka TAMISEMI katika Idara ya Serikali za Mitaa,anayefuata ni Bi.Sipora J.Liana Mkurugenzi wa Jiji la Dar Es Salaam,Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bwana Msongela  Palela na wa mwisho ni Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo Bwana Hetsoni Msalale Kipsi.Kikao hiki kilikuwa kinajadili mikakati mbalimbali ya namna gani ya kuliwezesha Shirika kufanya mabadiliko katika utendaji wake kuliko ulivyo hivi sasa, ambapo halionyeshi kufanya vizuri.

Sunday, November 13, 2016

Pilipili hoho ni mhimu kwa afya yako

Pilipili hoho ni miongoni mwa mazao maarufu sana yanayopatikana katika Soko Kuu la Kariakoo. Katika picha hapo juu ni Hoho njano na Nyekundu zote kwa pamoja zina manufaa tofauti kiafya kwa mlaji ukilinganisha na zile zenye rangi ya kijani ambazo zimezoeleka kwa watu wengi. Hoho hizi ni nadra sana kupatikana katika masoko ya kawaida, lakini hapa Sokoni Kariakoo ni maarufu sana kupatikana. Fika sokoni Kariakoo eneo la Shimoni katika Soko la Jumla utazipata Pilipili hizi kwa bei nzuri na ya kawaida. Kwa mahitaji ya Hotelini na majumbani.

Tuesday, October 18, 2016

Meneja Mkuu Mpya akutana na Watumishi wa Shirika

 Katika picha ni sehemu ya Watumishi wa Shirika la Masoko  Kariakoo wakiwa wanamsikiliza Meneja Mkuu mpya wa Shirika hili. Meneja Mkuu huyo mpya aliitisha mkutano huu ili aweze kujitambulisha kwa Watumishi wa Shirika. Bwana Hetson Msalale Kipsi pichani hayupo aliteuliwa rasmi na Mheshimiwa Rais Dk.John Magufuli tarehe 5 Septemba 2016 kuwa Meneja Mkuu Mpya wa Shirika hili. Bwana Kipsi kabla ya uteuzi huo alikuwa Mtumishi katika Wizara ya TAMISEMI, kwa taaluma yeye ni Mtaalam wa  Mambo ya Uchumi.
 Katika picha hapo juu ni Wajumbe wa Menejimenti ya Shirika la Masoko Kariakoo waliokaa mbele. Kutoka kushoto ni Meneja wa Fedha Bi.Marieta Masaua, Bwana Mathias Mbafu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, Bwana Donald T.Sokoni ambaye ni Meneja wa Afya na Usafi, Bwana Josam Mnzava ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama na Mlelo Mghen huyu ni Meneja Mipango na Biashara. Hawa pia walijumuika katika mkutano huu maalum uliokuwa na lengo la kumtambulisha Meneja Mkuu Mpya wa Shirika Bwana Hetson Msalale Kipsi.
 Meneja Utumishi na Utawala Bwana Godwin Mrosso aliyesimama, akizungumza kumkaribisha Meneja Mkuu Mpya wa Shirika  Bwana Hetson Msalale Kipsi aliyekaa katikati ili aweze kuzungumza na Watumishi wa Shirika na kujitambulisha kwa Watumishi hao. Mkutano huo ulifanyika ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Shirika ulioko katika Jengo Kuu la Soko kuu la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam.
 Bwana Denis Mfuruki aliyesimama katika picha hapo juu ambaye ni Mwenyekiti wa TUICO Tawi la Shirika la Masoko Kariakoo, akizungumza kumkaribisha Meneja Mkuu Mpya Bwana Hetson Msalale Kipsi ambaye amekaa. Bwana Mfuruki alimshukuru na kumpongeza  Meneja Mkuu huyo mpya kwa ujio wake kama Mtendaji Mkuu wa Shirika na kwamba Watumishi wapo tayari kushirikiana naye ili kuliletea Shirika maendeleo.
 Bwana Ncheye Kulwa aliyesimama ambaye kwa nafasi yake katika Utumishi katika Shirika  ni Mkaguzi wa Ndani,alikuwa miongoni mwa Watumishi waliopata nafasi yakumueleza Meneja Mkuu Mpya baadhi ya kero ambazo zinawasibu Watumishi. Bwana Ncheye Kulwa alieza kuhusu maslahi duni kwa Watumishi hasa kuhusu mishahara kuwa ni midogo sana na kumuomba Meneja Mkuu huyo mpya kuliangalia jambo hilo ili Watumishi wa Shirika wapate maslahi mazuri.
 Sehemu ya Watumishi wa Shirika la Masoko Kariakoo waliohudhuria Mkutano maalum huo wa Meneja Mkuu mpya kujitambulisha rasmi kwa Watumishi wa Shirika. Aliyesimama ni Bwana Nicodemas Mwakalindile yeye kama miongoni mwa Watumishi wa Shirika alimshukuru na kumpongeza Meneja Mkuu huyo mpya kwa kuteuliwa kwake kuwa Meneja Mkuu mpya wa Shirika la Masoko Kariakoo. Pia alitoa kero yake mbele ya Meneja Mkuu mpya ya kuwa ndani ya Taasisi hii upendo baina ya Watumishi wa kada ya chini na Menejimenti umepungua sana na kumuomba Meneja huyu mpya aweze kuirekebisha hali hiyo ili watumishi waweze kuwa na morali ya kufanya kazi.
 Katika picha hapo juu, aliyesimama ni Bi.Romana Lukanga, Mtumishi huyu mkongwe katika Shirika la Masoko Kariakoo.Kihistoria Mama huyu aliajiriwa Mwaka 1975, na wakati Soko Kuu la Kariakoo lilipokuwa linafunguliwa na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K.Nyerere yeye alishuhudia tukio hilo. Mtumishi huyu ombi lake kubwa kwa  Meneja Mkuu mpya ni kumtaka aboreshe maslahi ya Watumishi wote hasa wale wa kada ya chini ndani ya Shirika hili.Akizungumza kwa hisia Mtumishi huyu Bi.Lukanga alimwambia Meneja Mkuu kuwa yeye pamoja na wenzake wa kada yake wamekuwa katika hali duni kwakuwa mishahara yao ni midogo sanaa ukilinganisha muda ambao wamelitumikia Shirika.
 Katika picha hapo juu ni Bwana Mdami ambaye Mtumishi wa Shirika kutoka Kitengo cha Matunzo. Bwana Mdami naye alisisitiza juu ya kuboreshwa maslahi ya Watumishi. Akimuomba Meneja Mkuu mpya aweze kurekebisha hali duni ya mishahara kwa Watumishi wa Shirika.
 Meneja Mkuu mpya Bwana Hetson Kipsi akiwa amesimama kujibu baadhi ya hoja ambazo zilizungumzwa na Watumishi wa Shirika, pale alipotoa nafasi kwa Watumishi kuzungumza dukuduku zao. Pamoja na mengine Meneja Mkuu aliwaahidi Watumishi wa Shirika kwamba masuala yao yote yatafanyiwa kazi ipasavyo kwa kuzingatia Sheria,taratibu na kanuni za Utumishi ambazo zimewekwa kuliendesha Shirika hili.Akizungumza na Watumishi hao katika Ukumbi wa mikutano wa Shirika Meneja Mkuu alikiri kuwa zipo baadhi ya kero na changamoto ambazo alizifahamu tangu mapema hata kabla hajafika kuanza kazi rasmi ndani ya Shirika hili, hivyo basi Watumishi waondoe shaka na kwamba yeye amekuja kufanya kazi na kila Mtumishi kwa mujibu wa Sheria na kanuni za Shirika.
 Hapo juu katika picha ni Bwana Godwin Mrosso Meneja Utumishi na Utawala wa Shirika, akijibu baadhi ya hoja zinazohusu mambo ya Utumishi na Utawala. Bwana Mrosso alipewa nafasi hiyo yakutoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja ambazo Watumishi walizitoa mbele ya Meneja Mkuu aliyekaa katikati.
 Aliyesimama katika picha hapo juu ni Bwana Charles Sombe ambaye ni Afisa Utumishi Mwandamizi katika Shirika la Masoko Kariakoo. Afisa huyu alitoa ushauri kwa Meneja Mkuu huyo kuondoa makundi au matabaka ambayo yapo ndani ya Shirika kutokana na tofauti kadhaa wa kadhaa ili kujenga upya mshikano miongoni mwa Wafanyakazi wa Shirika.
Katika picha hapo juu ni Bwana Josam Mnzava  Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama akifafanua jambo katika mkutano Maalum wa Watumishi wa Shirika la Masoko Kariakoo. Mkutano huo uliokuwa na Agenda moja tuu ya Meneja Mkuu Mpya wa Shirika hilo Bwana Hetson Msalale Kipsi kujitambulisha na kuwatambua Watumishi wa Shirika hili rasmi tangu alipoteuliwa na Rais mwezi mmoja uliopita na kuanza kazi rasmi mapema mwanzoni mwa mwezi huu akiwa ametokea katika Wizara ya TAMISEMI iliyoko chini ya Ofisi ya Rais.

Sunday, October 2, 2016

MENEJA MKUU MPYA AKABIDHIWA OFISI -SHIRIKA LA MSOKO KARIAKOO SEPT.30,2016

 Picha hiiya pamoja ambayo inaonyesha tukio la kumkaribisha Meneja Mkuu mpya wa Shirika la Masoko Kariakoo siku ya Ijumaa tarehe 30.9.2016 mchana. Hafla hii fupi ilifanyika katika Ofisi za Shirika hili zilizopo katika Jengo Kuu la Soko Kuu la Kariakoo.Aliyeketi katika kiti ni Meneja Mkuu mpya wa Shirika Bwana Hetson Kipsi, na waliosimama kutoka kushoto ni Bwana Mlelo Mgheni Meneja Biashara na Mipango wa Shirika, Bwana Denisi Mfuruki ni Mjumbe wa Bodi ya Shirika,Bwana Cprian Kuyava kutoka Hazina ambaye pia  ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Bwana Dk. Buhohela Lunogelo ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika, Bwana Florens Seiya aliyekuwa Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko na sasa amemaliza muda wake wa Utumishi katika Shirika hili. Anayefuata ni Meneja Utumishi na Utawala wa Shirika Bwana Godwin Mroso, Bwana Mathias Mbafu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi katika Shirika,Meneja wa Fedha Bi.Marieta Masaua ambaye ni Meneja wa Fedha katika Shirika,Bwana Donald Sokoni Meneja wa Afya na Usafi,Bwana Josam Mnzava Mkuu wa Kitengo cha Usalama,Bwana Paul Kiwera Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi cha Ndani,na Bwana Flavian Mlelwa Kaim Mkuu wa Kitengo cha Matunzo.
 Wakati wa makabidhiano ya Ofisi  Dua na Sala fupi zilifanyika ndani ya Ofisi ya Meneja Mkuu kama ishara ya kumuombea mafanikio Meneja Mkuu aliyekuwa akimaliza muda wake na kadhalika kama ishara yakumuombea Meneja Mkuu mpya wa Shirika kupata ufanisi kiutumishi na hekima ya Mungu imuongoze katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mtumishi wa Umma mwenye kuwatumikia Watanzania.



 Meneja Mkuu mpya Bwana hetson Kipsi akizungumza na Menejimenti ya Shirika  pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Masoko Kariakoo katika kikao kifupi cha kukabidhiwa Ofisi. Meneja Mkuu huyo mpya alisisitiza ufanisi na uwazi pamoja na kujituma katika Utumishi ndani ya Menejimenti. Mambo hayo ya msingi ndiyo hasa yatakayo lisaidia Shirika hilo kupiga hatua ya kimaendeleo. Lakini alionya tabia ya uzembe kwa Watendaji wa Shirika jambo ambalo alisema hatalivumilia hata kidogo katika uongozi wake katika Shirika hili kongwe lililoanzishwa Mwaka 1974 kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Namba36, ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
 Meneja Mkuu  Bwana Florens Seiya aliyemaliza muda wakeakitoa hotuba fupi ya kuelezea mwenendo mzima wa Shirika mbele  ya Meneja Mkuu mpya Bwana Hetson Kipsi na Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Shirika hilo muda mfupi kabla ya makabidhiano ya ya Ofisi, Ijumaa tarehe 30.9.2016 mchana. Hafla ilyofanyika katika Ofisi za Soko kuu la Kariakoo Jijini Dar Es Salaam.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika Bwana Dk.Buhohela Lunogelo akipeana na  mkono wa na Meneja Mkuu aliyemaliza muda wake wa Utumishi katika Taasisi hii. Anayetazama kwa karibu hapo ni Bwana Hetson Kipsi Meneja Mkuu mpya wa Shirika. Mwenyekiti wa Bodi huyo alimshukuru Meneja Mkuu aliyemaliza muda wake wa Utumishi na kumtakia heri katika muda wake wa utumishi uliobakia katika kuutumikia Umma. Kadhalika alimkaribisha Meneja Mkuu Mpya Ofisini.Bwana Kipsi alikuwa Mtumishi katika Wizara ya TAMISEMI ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais.Meneja huyu mpya ni Mtaalam wa Uchumi kwa taaluma yake.
 Katika picha hapo juu ni moja ya Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Masoko Kariakoo Bwana Denis Mfuruki mwenye karatasi mkononi akipeana mkono na Meneja Mkuu mpya wa Shirika  hilo Bwana Hetson Kipsi kama ishara ya upendo kumkaribisha Mtendaji Mkuu huyo mpya katika Ofisi ya Meneja Mkuu. Aliyesimama kushoto ni Bwana Florens Seiya ambaye amemaliza muda wake wa kuhudumu katika Shirika hili, baada yakufanya kazi hapa katika kipindi cha miaka saba.Mabadiliko haya ya Uongozi yamekuja baada ya Uteuzi mpya alioufanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk.John Magufuli mapema mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.
Hapa katika picha ni Meneja Mkuu Bwana Florens Seiya akipeana mkono na Meneja Mkuu mpya wa Shirika la Masoko Kariakoo Bwana Hetson Kipsi. Mameneja hawa walipeana mikono Ofisini katika Ofisi ya Meneja Mkuu wakishuhudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Masoko, Makamu Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Menejimenti ya Shirika hili,siku ya Ijumaa tarehe 30.9.2016 mchana.

Tuesday, July 12, 2016

Karibuni Wafanyabiashara kwa Matangazo

Shirika la Masoko ya Kariakoo, sasa linakaribisha Wafanyabiashara wa aina zote kwa Matangazo ya Biashara zao. Kwa wale wafanyabiashara wa ndani ya Shirika wanahamasishwa zaidi kutangaza biashara zao!
Lakini pia Makampuni tofauti yanakaribishwa pia kutangaza na sisi katika Blog yetu hii! Kwa mawasiliano zaidi ili kupata nafasi piga namba za simu zilizopo katika Blog.

Ahsanteni sana na Karibuni

Thursday, February 4, 2016

Mazao yanayopatikana Soko Kuu la Kariakoo

Miongoni mwa mazao muhimu ambayo huuzwa katika Soko Kuu la Kariakoo ni pamoja na Nazi.Nazi ambazo huuzwa katika soko hili maarufu zinatoka sehemu mbalimbali hapa nchini.Mikoa ifuatayo Tanga,Morogoro na Pwani ni sehemu ambako nazi huzalishwa kwa wingi.Nazi hizi huuzwa kwa bei ya jumla na rejareja.

Tuesday, November 24, 2015

Mboga aina zote Kariakoo Sokoni

Katika picha hapo juu ni mfanyabiashara wa mazao ya mbogamboga akiwa na mteja katika meza yake.Katika soko hili kila aina ya mbogamboga hupatikana takribani mwaka mzima!

SOKONI KARIAKOO

 Eneo la shimoni katika Soko Kuu la Kariakoo ambako bidhaa mbalimbali huuzwa kwa bei ya jumla na rejareja, eneo hili kwa sasa limekuwa bora zaidi kimpangilio kwa wafanyabiashara na kufanyiwa marekebisho ya taa za umeme ambazo zimeongeza mwanga wa kutosha.

 Nafaka za aina mbalimbali zinapatikana katika Soko Kuu la Kariakoo,ukifika sokoni utazipata nafaka hizi katika eneo la Soko dogo lililopo pembezoni mwa Jengo la Soko Kuu.

Katika picha akina mama hawa wakiwa Sokoni Kariakoo wakiandaa maharage mabichi kwa kuyamenya maganda  ili waweze kuwauzia wateja wao. Katika eneo hili kwa sasa limeboreshwa kwani sio tena wanakaa chini badala yake wanatumia meza nzuri na bora kwa kuhifadhia bidhaa zao wakati wa kuuza. Karibu sokoni Kariakoo.

Thursday, October 22, 2015

Mazao katika Soko Kuu la Kariakoo - Dar Es Salaam

 Zabibu ni miongoni mwa bidhaa zinazopatikana hapa Soko Kuu la Kariakoo, Jijini Dar Es Salaam. Bidhaa hii huzalishwa kwa wingi  mkoani Dodoma
vitunguu  saumu na tangawizi pia huuzwa katika soko kuu la Kariakoo. 
Pilipili Hoho hupatikana katika Soko kuu la Kariakoo takribani mwaka mzima. Pilipili hoho  huingizwa katika soko hili zikitokea katika mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro,Pwani na Tanga.Kwa bei ya jumla na rejareja huuzwa sokoni hapa kuanzia mapema alfajiri hadi jioni.

Monday, August 24, 2015

Matukio katika Picha

 Katika picha hapo juu kutoka kulia ni Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo Bwana Florens Seiya, Mwenyekiti wa TUICO tawi Bwana Dennis Mfuruki aliyesimama na Bwana Henry Rwejuna ambaye ni Katibu wa TUICO tawi, kwa pamoja wakiwa wanaendesha mkutano wa wafanyakazi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo mwishoni mwa wiki iliyopita. Ni moja ya mikutano ya kawaida ambayo imekuwa inafanyika kwa nia ya kujenga na kuimarisha mahusiano baina wafanyakazi wa shirika na Mwajiri wao, wakilenga zaidi hali ya mwenendo mzima wa Shirika.
 katika picha hapo juu ni vitunguu maji ambavyo ni moja ya bidhaa zinazouzwa hapa katika soko  Kuu la Kariakoo jijini Dar Es Salaam.Vitunguu maji hivi hufikishwa sokoni Kariakoo vikiwa vinatoka mikoa mbalimbali ya Tanzania kama vile Mbeya,Arusha,Iringa na Singida.
Picha hiyo hapo juu inaonyesha sehemu tuu ya Watumishi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo wakiwa wametulia huku wakifuatilia maelezo ya Meneja Mkuu wa Shirika ,pichani hapo juu hayupo wakati wa mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Shirika mwishoni mwa wiki iliyopita.