Mapema leo alfajiri Soko Kuu la Kariakoo lilivamiwa na Kundi la Mgambo wa kutoka Manispaa ya Ilala linaloendesha zoezi la kusafisha Jiji la Dar Es Salaam na kufanya uharibifu mkubwa kama unavyoonekana katika picha hapo juu. Kitendo hiki kimeushitua Uongozi wa Shirika la Masoko pamoja na Wafanyabiashara ambao huendesha shughuli zao katika Soko hili.
Eneo lililovamiwa na kuharibiwa kabisa ni hilo linaloonekana katika picha hapo juu;lipo katikati ya Jengo Kuu lenye paa la miavuli kushoto na Soko Dogo kulia ambalo katika picha hapo lina rangi ya kijani eneo hilo ni maarufu kama Soko la Wazi.Uharibifu huu ambao umefanyika mapema leo alfajiri umewaacha Wajasiriamali wengi katika hali ya sitofahamu hatma yao; lakini zaidi umeliingiza Shirika la Masoko katika hasara ambayo ni kubwa kimapato.
Kwa mujibu wa ramani hiyo hapo juu Kiwanja ambapo Soko Kuu la Kariakoo lilipo ni Eneo hilo katika mgawanyo wa viwanja linaonekana lenye umbo la herufi L (Block 40) na kwa mujibu wa ramani hiyo ambayo imesainiwa na Wizara yenye dhamana na ardhi inaonyesha eneo hilo lililovamiwa na kuharibiwa linamilikiwa na Shirika la Masoko ya Kariakoo.
Eneo hili kwa wale watu wenye mazoea ya kufika katika Soko Kuu la Kariakoo kujipatia mahitaji bila shaka watakuwa wanalijua , huwapo Wafanyabiashara wengi wakiwemo akina Mama Wajasiriamali na Vijana ambao hudamka mapema kila siku na kufanya biashara zao! lakini ilikuwa ni tofauti kabisaa leo pale walipofika na kuona eneo hilo limeharibiwa na Wanamgambo hao wa Manispaa ya Ilala.